Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Doha na matarajio ya kubadili maisha ya wakazi duniani

Mkutano wa Doha na matarajio ya kubadili maisha ya wakazi duniani

Washiriki kutoka zaidi ya nchi 142 wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa kimataifa dhidi ya uhalifu na utawala wa kisheria unaoanza kesho huko Doha, Qatar.

Mambo yatakayoangaziwa na washiriki hao ni pamoja na vitisho vipya vya uhalifu vinavyoibuka na changamoto za kuimarisha utawala wa sheria ili usaidie kufanikisha maendeleo endelevu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Doha, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo Meja Jenerali Dkt. Abdullah Yusuf Al-Maal ameshukuru Umoja wa Mataifa na ofisi yake inayohusika na madawa na uhalifu, UNODC kwa ushirikiano ili kongamano hilo liweze kufanikiwa.

Naye Katibu wa mkutano huo Jo Dedeyne-Amman, amesifu jitihada za mwenyeji Qatar kwa maandalizi mazuri.

“Ajenda ya mkutano huu inahusisha maudhui yanayogusa maisha ya wakazi duniani kote kama vile ujumuishaji na ushughulikiaji wa watuhumiwa, biashara haramu ya binadamu, usafirishaji haramu wa wahamiaji, aina mpya za uhalifu kama vile uhalifu mtandao pamoja na usafirishaji haramu wa mali za kitamaduni na mazao ya porini.”