Ban afungua mkutano wa ukanda wa Amerika, akutana pia na marais wa Cuba na Dominica
Umoja wa Mataifa umepongeza uongozi wa Rais Barack Obama wa Marekani na Raul Castro wa Cuba wa kuamua kurejesha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Saba wa viongozi wa nchi zilizo ukanda wa Amerika kwenye mji wa Panama,nchini Panama.
Amesema kitendo hicho kinaenda samamba na lengo la katiba ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuendeleza uhusiano mwema baina ya majirani, sanjari na wito wa muda mrefu wa nchi wanachama wa Umoja huo wa kutaka kurejeshwa kwa uhusiano huo uliokoma zaidi ya miongo mitano iliyopita.
Ban amesema uwepo wa Rais Obama na Rais Castro kwenye mkutano huo ni matamanio ya muda mrefu ya nchi zilizopo ukanda huo wa Amerika.
Hata hivyo Katibu Mkuu amesema ni matarajio yake kuwa nchi 35 wanachama wa ukanda huo wa Amerika wataendelea kutumia mashauriano kumaliza tofauti ndani ya nchi na baina ya nchi zao akisema hiyo ni muhimu siyo tu katika kuimarisha amani bali pia demokrasia.
Katibu Mkuu pia amezungumzia masuala ya utokomezaji umaskini na usawa akipongeza nchi hizo kwa harakati zao za kutokomeza umaskini huku akitaka zitumie jitihada hizo hizo kutokomeza ukosefu wa usawa na uwiano katika jamii.
Kando mwa mkutano huo, Ban amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Dominica Danilo Medina.
Katika mazungumzo hayo Bwana Ban amempongeza Rais Medina kwa kuwa mfano katika masuala mathalani elimu na ushirikiano baina ya nchi za kusini ambazo ni zile zinazoendelea.
Katibu Mkuu pia amekaribisha majadiliano kati aya Dominica na Haiti. Viongozi hao pia wamejadili kuhusu uraia, na uhamiaji pamoja na kulinda haki za za binadamu.
Halikadhalika Ban amekuwa na mazungumzo na Rais Raúl Castro, wa Cuba ambapo wamejadiliana mambo kadhaa ikiwemo mchango wa Cuba kwa kwenye jitihada za kimataifa za kutokomeza Ebola na kumkaribisha Rais Castro kwenye mkutano wa viongozi wa wakuu wa nchi wanachama utakaojadili ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.
Mkutano huo utafanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mwezi Septemba mwaka huu.