Skip to main content

Mzozo wa kidini Yemen waweza kuenea kwenye ukanda mzima: Washauri

Mzozo wa kidini Yemen waweza kuenea kwenye ukanda mzima: Washauri

Washauri maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali inavyozidi kuzorota nchini Yemen kila uchao wakisema kuna hatari mvutano wa kidini baina ya pande husika ukasambaa kwenye ukanda mzima.

Adama Dieng, mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari na Jennifer Welsh anayehusika na wajibu wa kulinda wamesema hayo katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo jijini New York.

Mathalani wamegusia operesheni za kijeshi nchini Yemen zinazofanywa na nchi za ukanda huo zikiongozwa na Saudi Arabia kufuatia ombi la serikali ya Yemen.

Bwana Dieng na Bi, Welsh wameeleza wasiwasi wao pia kuhusu ongezeko la mashambulizo yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Qaeda kwenye rasi ya Arabia, AQAP na kundi la Houthi sanjari na vikundi vyenye ushirika nao.

Wamestaajabu vile ambavyo makundi yanayopaswa kulindwa kama vile wahudumu wa afya, raia wakishambuliwa, huku maeneo ya kutoa huduma, makazi na shule yakisambaratishwa.

Wamekumbusha pande husika kwenye  mzozo huo umuhimu wa kulinda makundi hayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa wakisema mashambulizi dhidi yao yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Wamerejelea wito wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon kwa pande zote kuwajibika kwa mujibu wa sheria za kibinadamu  za kimataifa.