Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changisho la dharura kusaidia wakimbizi wa Nigeria lawekwa hadharani

Changisho la dharura kusaidia wakimbizi wa Nigeria lawekwa hadharani

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya kiserikali yanazindua changisho maalum la zaidi ya dola Milioni 174 kwa ajili ya kushughulikia madhila yanayokumba wakimbizi wa Nigeria kwenye ukanda wa Afrika Magharibi, likijulikana kama RRRR.

Fedha hizo ni kwa ajili ya wakimbizi 192,000 waliokimbia Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria kutokana na mashambulizi yanayofanywa na magaidi wa Boko Haram kwenye eneo hilo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema changisho hilo la dharura ni linasaka misaada ya kuokoa maisha kwa raia wa Nigeria 74,000 waliosaka hifadhi Kaskazini mwa Cameroon, halikadhalika 18,000 kusini-magharibi mwa Chad na wengine waliokimbilia Niger.

Mwakilishi wa UNHCR huko Afrika Magharibi Liz Ahua amesema wakimbizi hao wako katika mazingira magumu huku wakigubikwa na hofu na woga na sasa hawawezi kurejea nyumbani.

Hivyo amesema wanahitaji zaidi msaada huo wa kifedha ili kuwapatia  usaidizi na hata kuweka mipango ya baadaye iwapo watu wengine watazidi kusaka hifadhi nje ya Nigeria kwa ajili ya usalama wao.