Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalamu wa UM ataka usalama kwa walio katika mazingira hatarishi Kazakhstan

Mtalamu wa UM ataka usalama kwa walio katika mazingira hatarishi Kazakhstan

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na vitu vyenye madhara na taka, ameitaka serikali ya Kazakhstan kuchukua hatua muhimu kuwalinda raia wake wanaoishi katika maeneo yaliyohatarishi kimazingira. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya John Kibego)

Picha:: UN Photo/F ChartonAkiongea baada ya ziara rasmi nchini humo, Baskut Tuncak amesema, ingawa serikali imechukua hatua chanya ikiwemo kuheshimu mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira ili  kudhibiti athari ya vitu vyenye sumu na taka, ameshuhudia watu waliozungukwa na milima ya taka yenye sumu na miji iliogubikwa na hewa chafu.

Ameongezea kwamba amepata taarifa za uwepo wa sehemu haramu za kutupa taka zenye sumu na mionzi hatari.

Katika ziara hiyo ya siku 14, ameongea na wakazi ambao wamechanganyikiwa wakipumua hewa chafuzi, wakinywa maji na vyakula vichafu huku wengine wakisubiri kuhamishwa.

Magonjwa mengi miongoni mwa watu hao yamehusishwa na viwanda, machimbo ya madini na taka na mionzi hatari.

Amesisitiza kuwa lazima serikali ya Kazakhstan ishughulikie tatizo hilo kwani watu hawataendelea kuishi katika hofu.

Mjumbe huyo Maalumu anatarajiwa kutoa ripoti kuhusu nchi hiyo kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi September mwaka huu.