Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wa chakula ni msingi wa afya na maendeleo duniani

Usalama wa chakula ni msingi wa afya na maendeleo duniani

Athari zitokanazo na ukosefu wa usalama wa chakula zinaweza kuathiri sekta ya uchumi na uzalishaji wa chakula kwa ujumla, amesema Naibu Rais wa Baraza Kuu Nicholas Emiliou, ambaye pia Mwalikishi wa Kudumu wa Cyprus kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza katika mkutano maalum kuhusu usalama wa chakula uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Afya duniani WHO na Shirika la Chakula na Kilimo FAO wakati wa maadhimisho ya siku ya afya duniani, ulikuwa na lengo la kujadili uhusiano kati ya afya, maendeleo na usalama wa chakula.

Katika ujumbe wake alioutoa kwa niaba ya rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa, Balozi Emiliou amesema watu milioni 2 wanafariki duniani kila mwaka kutokana na magonjwa yanayoletwa na vyakula au maji, kwa hiyo usalama wa chakula ni jambo la muhimu sana.

“ Magonjwa mengi yatokanayo na vyakula yanaweza kuzuiliwa kupitia utaratibu salama wa kugusa vyakula. Kufuatilia sheria za usalama wa chakula kama kunawa mikono, kusafisha na kuondoa vijidudu kwenye sehemu za kupikia kunaweza kuimarisha usalama wa chakula. Jitihada zote zinahitajika ili kuzuia uwepo wa magonjwa yatokanayo na vyakula kwa ajili ya uzima wa watu, familia na jamii”

Naibu Rais huyo wa Baraza Kuu ameongeza kwamba usalama wa chakula ni muhimu katika kupambana na utapiamlo na umaskini.

Kwa mujibu wa WHO, ukosefu wa usalama wa chakula ni chanzo cha zaidi ya aina 200 za magonjwa, yakiwemo kuhara, mafua ya ndege na minyoo.