Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wawili wajeruhiwa na bomu la kutegwa ardhini Mali

Walinda amani wawili wajeruhiwa na bomu la kutegwa ardhini Mali

Walinda amani wawili wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, wamejeruhiwa baada ya gari lao kupita juu ya bomu la kutegwa ardhini, kilomita 30 kutoka mji wa Kidal, kaskazini mwa nchi hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa leo, MINUSMA imesema walinda amani hao wamepelekwa kwenye hospitali ya Gao ili kupatiwa matibabu.

MINUSMA imelaani vikali kitendo hicho ilichokiita cha ugaidi, ikisema kinalenga kukwamisha operesheni zake kwenye maeneo hayo ya Mali na kuumiza wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa au raia wa kawaida.

Aidha MINUSMA imesema inaendelea kutafuta, kutambua na kusafisha maeneo ambapo mabomu yametegwa ardhini, kwa ushirikiano na chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusiana na swala hilo, UNMAS, ili kulinda raia wa Mali.