Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO, UNICEF zajitutumua kutokomeza Surua Sudan

WHO, UNICEF zajitutumua kutokomeza Surua Sudan

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, na lile la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, kwa kushirikiana na serikali ya Sudan na wadau wengine wanaendelea kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa surua katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa nchini humo. Assumpta Massoi na maelezo kamili.

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Takribani visa 1600 vinakadiriwa huku 710 vikithibitishwa kutoka maeneo 23 katika majimbo 12 ya Sudan tangu mlipuko wa surua uanze mwezi Desemba mwaka jana .

Miongoni mwa majimbo yalioathirika zaidi ni Darfur Magharibi ambapo visa vingi vimeripotiwa kwa wafanyakazi migodini. Halikadhalika hivi karibuni visa vipya vimeripotiwa Kaskazini mwa Darfur eneo ambalo limegubikwa na wakimbizi wa ndani.

Tangu kuanza kwa mlipuko wa surua juhudi mbalimbali zimefanyika kuudhibiti ugonjwa huo ikiwamo kuendesha kampeni ya utolewaji wa chanjo ambapo katika maeneo tofauti zaidi ya watoto 10000 wamechanjwa.