Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNRWA aliomba baraza la usalama lifikie makubaliano juu ya Yarmouk

Mkuu wa UNRWA aliomba baraza la usalama lifikie makubaliano juu ya Yarmouk

Kamishna Mkuu wa Shirika La Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA, Pierre Krahenbuhl amesema kwamba leo amewaelezea wanachama wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu kuhusu hali ya kibinadamu katika kambi ya wakimbizi ya Yarmouk.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Jerusalem, akieleza kwamba hali inazidi kuwa tete kwa wakimbizi wa Palestina wanaoishi kwenye kambi hiyo ambayo imezingirwa na mapigano kwa miaka miwili.

Bwana Krahenbuhl amesema ametembelea kambi ya Yarmouk wiki tatu zilizopita na ameshuhudia hali mbaya ya njaa, wazee, wanawake na wajawazito wakiathirika zaidi, kwa sababu mashirika ya kibinadamu yanashindwa kufikisha misaada kwenye kambi hiyo kutokana na mapigano.

Ametoa wito kwa pande husika katika mzozo kuheshimu maisha ya raia na kwa jamii ya kimataifa kushirikiana zaidi, akieleza kwamba mpaka sasa hivi, nchi wanachama wa baraza la usalama hawajakubaliana juu ya swala hilo.

“Tunaamini kwamba hatua za pamoja kutoka kwa wanachama wa baraza la usalama na nchi wanachama za Umoja wa Mataifa zinahitajika kwa haraka ili kutekeleza mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuhakikisha haki za binadamu na sheria zaa kibinadamu zinaheshimiwa. Pia mimi binafsi naamini kwamba hali ya Yarmouk ni fursa kwa jamii ya kimataifa kufanya kazi zaidi kwa pamoja ili kukabiliana na mahitaji yaliyipo pale.”