Skip to main content

Rais Kikwete kuongoza jopo la kimataifa la kuhusu masuala ya afya

Rais Kikwete kuongoza jopo la kimataifa la kuhusu masuala ya afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunda jopo la dunia la kuchukua hatua juu ya majanga ya afya ambapo amemteua Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kuwa mwenyekiti wake.
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq ametaja wajumbe wa jopo hilo kuwa ni pamoja na Celso Luiz Nunes Amorim wa Brazil, Micheline Calmy-Rey wa Uswisi, Marty Natalegawa wa Indonesia, Joy Phumaphi wa Botswana na Rajiv Shah wa Marekani.
Katibu Mkuu ameliomba jopo hilo kutoa mapendekezo yatakayoweza kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa ili kuzuia na kushughulikia majanga ya afya yanayoweza kujitokeza, kwa kuzingatia yale yaliyojitokeza kwenye mlipuko wa Ebola.
Kwa mantiki hiyo jopo hilo litafanya mashauriano ya kina ikiwemo na wawakilishi wa nchi zilizoathiriwa na Ebola, jamii na Umoja wa Mataifa, bila kusahau mashirika ya kifedha na yale ya kikanda na yasiyo ya kiserikali.
Mkutano wa kwanza wa jopo hilo unatarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka 2015 na linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu mwezi Disemba mwaka huu na hatimaye Katibu Mkuu ataiwasilisha Baraza Kuu.