Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Yemen, wajumbe wanafikiria pendekezo la kusitisha mashambulizi

Mzozo Yemen, wajumbe wanafikiria pendekezo la kusitisha mashambulizi

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanafikiria rasimu ya azimio lililowasilishwa na Urusi ambalo linatolea wito wa kusitisha mashambulizi kwa muda huko Yemen ili huduma za kibinadamu ziweze kusambazwa.
Hiyo ni kwa mujibu wa Rais wa Baraza hilo Balozi Dinar Kawar wa Jordan alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, siku ya Jumamosi baada ya mashauriano ya faragha baina ya wajumbe siku ya Jumamosi.
Kikao hicho cha faragha kiliitishwa kufuatia ombi la Urusi ambapo Balozi Kawar amesema wajumbe wanahitaji kufikiria pendekezo hilo la Urusi lililowasilishwa wakati huu nchi jirani na Yemen zikiongozwa na Saudi Arabia zinafanya mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya Houthi.
"Wajumbe wa Baraza pia wamesisitiza wasiwasi wao kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu Yemen. Ujumbe wa Urusi umesambaza rasimu ya azimio kwa wajumbe wa baraza kuhusu usitishaji wa mapigano Yemen na kuelezea hofu yao hali mbaya ya kibinadamu kwa muda sasa nchini Yemen. Wajumbe wa Baraza wanahitaji muda kufikiria pendekezo hilo la Urusi.”