Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lalaani shambulio la kigaidi Kenya

Baraza la usalama lalaani shambulio la kigaidi Kenya

Wajumbe wa baraza la usalama wamelaani na kueleza masikitiko yao kufuatia shambulio la kigaidi lililotekelezwa nakundila kigaidi Al Shabaab huko Garissa nchini Kenya.

Wajumbe wametuma salamu zao za rambirambi kwa familia, waathiriwa, watu na seriakli ya Kenya huku wakiwatakia uponyaji wa haraka waliojeruhiwa katika shambulizi hilo.

Katika taarifa yao Ijumaa hii wametambua juhudi za Kenya katika kupambana na ugaidi pamoja na jukumu la nchi hiyo katika Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) katika makabiliano dhidi ya Al shabaab.

Pia wajumbe hao wamesema ugaidi bila  kujali aina yake na udhihirisho wake unasalia kuwa moja ya vitisho vikuu kwa amani na usalama wa kimataifa na kwamba vitendo vyovyote vya ugaidi ni uhalifu na havikubaliki bila kujali sababu, eneo na muda au nani katekeleza.

Wamesisistiza adhma yao ya kupambana na aina zote za ugaidi kwa mujibu wa kanuni za mkataba wa Umoja wa Mataifa na kutaka watekelezaji, waandaji, na wadhamini wa  shambulio hilo la ugaidi nchini Kenya kufikishwa katika vyombo vya sheria.