Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza kufikiwa mkakati wa nyuklia na Iran

Ban apongeza kufikiwa mkakati wa nyuklia na Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amepongeza nchi zilizohusika katika mazungumzo ya kufikia mkakati wa kisiasa unaoweka barabara ya kuafikia mpango wa pamoja wa kina wa kuchukua hatua, unaotarajiwa ifikapo tarehe 30 Juni 2015. Nchi zilizoshiriki mazungumzo hayo ni Marekani, Uchina, Urusi, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Iran kwa upande mwingine.

Taarifa ya msemaji wa Ban imemnukuu akisema kwamba mkataba huo wa kina utaweka mipaka kwa uwezo wa mpango wa Iran wa nishati ya nyuklia na kuondolewa kwa vikwazo. Mkataba huo pia utaheshimu mahitaji na haki za Iran, huku ukitoa hakikisho kwa jamii ya kimataifa kwamba shughuli zake za nyuklia zitaendelea kuwa za amani pekee.

Katibu Mkuu anaamini kwamba suluhu la kina litokanalo na mazungumzo kuhusu suala la nyuklia Iran, litachangia amani na ustawi ya kikanda, na kuwezesha nchi zote kushirikiana haraka ili kukabiliana na changamoto kubwa za usalama zinazozikumba.