Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandamano Mali, MINUSMA ilitumia nguvu bila kibali:Ripoti

Maandamano Mali, MINUSMA ilitumia nguvu bila kibali:Ripoti

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameomba radhi kufuatia maandamano yaliyoghubikwa na ghasia ambayo yalifanyika tarehe 27 Januari mwaka huu huko Gao, Mali mbele ya ofisi za ujumbe wa umoja huo, MINUSMA.

Tamko hilo la Ban linafuatia ripoti iliyowasilishwa kwake hii leo na jopo alilounda kuchunguza tukio hilo lililosababisha vifo vya raia wanne na wengine watatu walijeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amenukuu ripoti hiyo pia ikitaja ushiriki wa waandamanaji katika ghasia hiyo ikiwemo kurusha vilipuzi na chupa kwenye ofisi za MINUSMA. Hata hivyo..

(Sauti ya Farhan)

"Katibu Mkuu ana masikitiko makubwa kutokana na wahanga miongoni mwa raia kufuatia matumizi ya nguvu kupita kiasi kulikofanywa na watendaji wa MINUSMA. Amelaani vikali akisema huo ni ukiukwaji wa kanuni za utumiaji nguvu za MINUSMA.”

Akaenda mbali zaidi..

“Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu anaomba radhi ya dhati kwa wahanga na familia.”

Umoja wa Mataifa umesihi serikali ya Mali kuzingatia wajibu wake kwenye utendaji wa MINUSMA ambapo Katibu Mkuu amesema anahakikisha Umoja wa Mataifa kwa unawajibisha waliohusika huku ikichukua hatua kuhakikisha jambo hilo halitokei tena..