Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Indonesia yaambiwa isiwauwe wahalifu wa madawa ya kulevya

Indonesia yaambiwa isiwauwe wahalifu wa madawa ya kulevya

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imeishutumu Indonesia kwa kushindwa kuitikia wito wa kamati hiyo mwaka 2013, wa kutaka nchi hiyo ikomeshe mauaji ya wafungwa kwa makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya.

Baada ya tathmini ya mara kwa mara ya hali ya haki za binadamu nchini Indonesia, kamati hiyo ilitoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kurejesha sitisho la kutekeleza hukumu ya kifo, na kuhakikisha kuwa iwapo hukumu hiyo ingetumiwa, iwe tu kwa uhalifu mbaya sana, ambao haujumuishi ule unaohusiana na madawa.

Ikisikitishwa na kwamba Indonesia haijabadili sheria yake kama ilivyoombwa kufanya, Kamati hiyo iliipa Indonesia alama E, ambayo ndiyo ya chini zaidi katika tathmini ya hali ya haki za binadamu katika nchi yoyote ile.

Kamati hiyo pia imeitaka Indonesia ifanyie marekebisho sheria yake ili makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya yasiadhibiwe kwa adhabu ya kifo.