Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati ya Haki za Binadamu yaitaka Urusi itimize wajibu wake

Kamati ya Haki za Binadamu yaitaka Urusi itimize wajibu wake

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imeitaka serikali ya Urusi itimize wajibu wake chini ya Sheria ya Haki za Binadamu, kwa kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa katika kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria ya haki za binadamu, ambavyo vinatekelezwa na makundi yenye silaha na mamlaka zilizojitangaza katika maeneo ya Donetsk, Luhansk na Ossetia Kusini, kwani tayari Urusi ina ushawishi mkubwa dhidi ya makundi na mamlaka hizo.

Aidha, Urusi imetakiwa ifanye uchunguzi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika jimbo la Caucusus Kaskazini, na kuwawajibisha maafisa wa usalama wa serikali wanaodaiwa kufanya mauaji, utekaji nyara, utesaji na vizuizi vya siri na adhabu za kujumlisha dhidi ya washukiwa na familia za watu wanaodaiwa kuunga mkono washukiwa wa vitendo vya kigaidi.

Kuhusu ubaguzi wa rangi na chuki za kikabila, Kamati imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuwepo kwa vitendo vya kibaguzi, ukiwemo uhalifu unaochochewa na ubaguzi wa rangi, kama vile mashambulizi ya wanadoria wa Cossack dhidi ya watu wasio wenye asili ya Slav, wakiwemo wahamiaji Asia ya Kati, Caucasus, Afrika na Roma, na kuitaka serikali ya Urusi ifanye juhudi zaidi kukabiliana na vitendo vya ubaguzi.

Kamati imeelezea wasiwasi wake pia kuhusu kuenea kwa makundi yenye msimamo mkali, yakiwemo yale yenye hisia kali za utaifa, makundi yanayoandama chuki za Ki-Nazi na matumizi ya lugha ya ubaguzi katika hotuba za kisiasa, mathalan kampeni za uchanguzi na katika vyombo vya habari dhidi ya makundi ya walio wachache.