Skip to main content

Vita dhidi ya FDLR vinahitaji msaada wa MONUSCO, asema Kobler

Vita dhidi ya FDLR vinahitaji msaada wa MONUSCO, asema Kobler

Operesheni dhidi ya waasi wa FDLR nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, zinazotekelezwa na jeshi la jitaifa, FARDC, zinahitaji usaidizi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO.

Hii ni kwa mujibu wa Martin Kobler, mkuu wa MONUSCO, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa baada ya kuhitimisha ziara yake katika maeneo ya Kivu Kaskazini, wiki iliyopita.

Amesema, operesheni za FARDC zina kasoro zao na anahisi kwamba ni lazima kurejesha usaidizi wa MONUSCO haraka iwezekanavyo.

Umoja unaleta nguvu. Tuko na uwezo, tuko na vyakula, tuko na uwezo wa kupigana, pamoja na FARDC. Ni maswala nimeyazungumzia na serikali na naamini sana kwamba tutapata suluhu. Ili kuondoka nchini, tunapaswa kutengeneza hali bora ya usalama. Tukishirikiana kwa haraka na FARDC, ndio tutaweza kupunguza idadi ya walinda amani wa ujumbe huo” .

Operesheni dhidi ya FDLR zilipoanza, serikali ya DRC ilitangaza kutohitaji tena usaidizi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa baada ya MONUSCO kukataa kushirikiana na majenerali wawili ambao wametuhumiwa kwa kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu.