Skip to main content

Tuwapatie fursa wenye usonji wachangie katika jamii zao: Ban

Tuwapatie fursa wenye usonji wachangie katika jamii zao: Ban

Ikiwa leo ni Siku ya Usonji Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa anatiwa moyo sana na ongezeko la uelewa wa jamii, pamoja na kuimarishwa kwa huduma kwa watu wanaoishi na hali hiyo. Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Katika ujumbe wake wa siku hii, Ban amesema kuhamasika kwa jamii kuhusu usonji siyo tu kunaongeza uelewa bali pia kunapatia wazazi uwezo wa kusaka tiba ya hali hiyo.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa ujumuishaji katika jamii kwa kundi hilo, mathalani watunga sera kushawishi shule kuandikisha watoto wenye usonji ili waweze kupata elimu ndani ya jamii zao.

Ban amesema kuwa yeye na mkewe Yoo Soon-taek, wanazindua mchakato wa kuchukuwa hatua, wakitoa wito kwa waajiri kuwapa ajira watu wenye usonji

“Siku hii ya Usonji Duniani, familia yangu inashikamana na wote walioathiriwa. Tuunganishe juhudi zetu ili tuweke mazingira bora zaidi kwa watu wenye usonji, ili waweze kuchangia mustakhbali ambao ni wa haki na endelevu kwa wote.”

Nchini Tanzania maandamano yamefanyika leo kwenye wilaya Saba za mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuhamasisha uelewa juu ya Usonji, na Grace Lyimo Rais na Mkurugenzi wa taasisi ya Autism Connects Tanzania anaelezea kiwango cha uelewa kwa sasa.

(Sauti ya Grace)