Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wahanga wa mzozo wa Yemen : Zerrougui

Watoto wahanga wa mzozo wa Yemen : Zerrougui

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto vitani, Leila Zerrougui, leo amezisihi pande zote kwenye mzozo wa Yemen kulinda haki za watoto nchini humo. Katika taarifa yake, Bi, Zerrougui amenukuliwa akisema kutishiwa na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watoto Yemen, akisema watoto hao wanahitaji ulinzi kwa haraka.

Wakati huo huo, mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Yemen, Johannes Van Der Klaauw amelaani mauaji ya mfanayakazi wa kujitolea wa Shirika la Hilali nyekundu la Yemen, kusini mwa nchi, siku ya jumatatu.

Bwana Van Der Klaauw ametoa wito kwa pande zote za mzozo kuhakikisha wafanyakazi wa kibinadamu wanaweza kusafiri na kufikisha jamii ambazo wanahitaji msaada bila kizuizi, pamoja na kusafirisha vifaa vya misaada.

Aidha amesikitishwa na kiwango cha uharibifu na idadi ya vifo nchini humo, akiongeza kwamba raia wote wa Yemen watakuwa hatarini iwapo suluhisho la kisiasa haliyapatiwa.

Kwa mujibu wa UNICEF,  kwa kipindi cha wiki moja tu, tayari watoto 62 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa, huku wengine wakitumikishwa vitani na makundi ya waasi.