Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na serikali kurejesha usalama wa chakula nchini Mali

FAO na serikali kurejesha usalama wa chakula nchini Mali

Familia 33,000 zilizoathiriwa na vita na mabadiliko ya tabianchi kaskazini mwa Mali zitapewa misaada kupitia mradi mpya wa kurejesha uzalishaji wa kilimo.

Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO na serikali ya Mali zimezindua leo utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya dola Milioni Tano.

Katika taarifa iliyotolewa leo, FAO imesema kilimo kimeathirika na mzozo unaoendelea kaskazini mwa nchi, pamoja na ukame na mafuriko yanayoathiri eneo hilo kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.

Mradi huo unalenga familia 25,000 ambazo zitasaidiwa kuanza upya kilimo cha mazao na maua, na nyingine 8,000 zinazotegemea mifugo ambazo zitasaidiwa vyakula na matibabu kwa mifugo kwenye maeneo ya Gao, Mopti na Timbuktu.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva, amesema mradi huo utachangia katika utaratibu wa amani nchini humo kwa sababu usalama wa chakula na usalama vina uhusiano mkubwa.

Mradi huo wenye thamani ya dola Milioni 100, ni sehemu ya mradi wa Benki ya Dunia wa kujenga upya Mali.