Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepushe Iraq dhidi ya mzozo wa kidini: Ban

Tuepushe Iraq dhidi ya mzozo wa kidini: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York ambapo wamejadili suala la Yemen, Iraq na Syria.

Kuhusu Yemen Ban amekaririwa akielezea ugumu wa hali ya kibinadamu nchini humo inayozidi kudorora kutokana na mapigano yanayosababisha wahitaji washindwe kufikiwa.

Kwa upande wa Iraq, viongozi hao wamejadili umuhimu wa nchi zote kwenye eneo hilo kuhakikisha Iraq haitumbukii kwenye mzozo wa kidini.

Ban ameisihi Iran ifanye kila iwezalo kusaidia jitihada za serikali ya Iraq za kuendeleza maridhiano ya kitaifa.

Kuhusu Syria, Ban na Naibu Waziri Abdollahian wamejadili jinsi ya kuendeleza mashauriano, chombo cha mpito cha utawala na kumaliza mzozo na hatimaye machungu yanayokabili wananchi wa Syria.