Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yakaribisha Palestina kama mwanachama mpya

ICC yakaribisha Palestina kama mwanachama mpya

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai, ICC, leo imefanya halfa ya kulikaribisha taifa la Palestina kama nchi mwanachama wa 123 wa Mkataba wa Roma, ambao ulianzisha mahakama hiyo.

Wakati wa hafla hiyo iliyofanyika mjini The Hague, Uholanzi, Makamu wa pili wa Rais wa ICC, Jaji Kuniko Ozaki, ameiwasilisha nakala maalum ya Mkataba wa Roma, kama ishara ya ahadi ya pamoja ya kudumisha utawala wa sheria.

(Sauti ya Jaji Ozaki)

“Kuridhia mkataba, bila shaka, ni hatua ya kwanza tu. Mkataba wa Roma unapoanza kutekelezwa leo na taifa la Palestina, Palestina inapata haki zote na wajibu unaotokana na kuwa mwanachama wa mkataba huu. Huu ni wajibu muhimu ambao hauwezi kuchukuliwa hivi hivi tu.”

Akiipokea nakala hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Dkt. Riad Al-Malki naye akasema:

(Sauti ya Dkt. Riad)

“Palestine inapokuwa rasmi mwanachama wa Mkataba wa Roma hii leo, ulimwengu umepiga hatua moja katika kukaribia kumaliza kutowajibika kwa uhalifu na udhalimu wa muda mrefu. Ama kweli, siku hii inatuleta karibu zaidi na malengo yetu ya pamoja ya haki na Amani.”

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na rais wa Baraza la nchi wanachama wa Mkataba wa Roma, Sidiki Kaba, majaji wa ICC na Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu, James Stewart.