Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ampongeza Buhari, rais mteule Nigeria

Ban ampongeza Buhari, rais mteule Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amempongeza Muhammadu Buhari ambaye amechaguliwa kuwa rais mpya wa Nigeria. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Ban ameelezea kupokea matokeo ya uchaguzi wa urais wa ubunge yaliyotolewa jana na tume huru ya kitaifa ya uchaguzi.

Amesema pia kuwa amezungumza na rais anayeondoka, Goodluck Ebele Jonathan, na mshindi wa uchaguzi, Meja Jenarali Muhammadu Buhari, akimpongeza rais Jonathan kwa uongozi wake wakati wa utaratibu wa uchaguzi.

Halikadhalika Bwana Ban ameipongeza tume ya uchaguzi kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi licha ya hali tete nchini humo, akiongeza kuwa yameonyesha ubora wa demokrasia nchini Nigeria.

Katibu Mkuu amewaomba Wanigeria wote wakubali matokeo ya uchaguzi na watumie njia za kisheria kuwasilisha malalamiko yao.