Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania ibadili sheria za kimila zinazonyanyapaa mwanamke: watalaam wa UM

Tanzania ibadili sheria za kimila zinazonyanyapaa mwanamke: watalaam wa UM

Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake, CEDAW, imetoa wito leo kwa Tanzania ibadili sheria za kimila zinazonyanyapaa wanawake.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema wito huo umetolewa baada ya kamati hiyo kuzingatia malalamiko ya wajane wawili ambao wamekataliwa kurithi mali za waume zao na kufukuzwa kwenye nyumba na wakwe wao.

Wanawake hao wawili wakitambulika kwa majina E.S na C.S walifungua madai yao mwaka 2005 wakisema sheria hizo za kimila ni kinyume na Katiba ya Tanzania, halikadhalika mkataba wa CEDAW ambao Tanzania imeridhia.

Halikadhalika walidai kuwa mamilioni ya wanawake wananyanyapaliwa na sheria za mila ambazo zinatekelezwa kwenye wilaya 30 za Tanzania.

Mwaka 2006, mahakama kuu ya Tanzania iliamua kutopindua sheria hizo ikisema itafungua njia kwa mila za makabila yote 120 ya Tanzania na kesi zitakuwa nyingi.

Uamuzi uliochukuliwa na CEDAW ni kuiomba Tanzania iweke mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake mbele ya sheria za kimila, na kuwafundisha majaji kuhusu swala hilo. Tanzania imepewa muda wa miezi sita kujibu maombi hayo.