Skip to main content

Ukatili wa Boko Haram ukomeshwe: Zeid

Ukatili wa Boko Haram ukomeshwe: Zeid

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao maalum huko Geneva, Uswisi kilichoangazia ukatili unaofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram huko Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria na nchi jirani.

Akihutubia kikao hicho Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kile kilichoanza kama mgogoro wa eneo dogo sasa kimetanuka na kusababisha zahma kwenye ukanda mzima, akitaka ukatili uliokithiri wa kundi hilo uchukuliwe hatua za kisheria.

Ametolea mfano mauaji, wanawake na watoto wa kike hadi wenye umri wa miaka 12 kutekwa nyara na kufanyiwa ukatili wa kutisha ikiwemo ule wa kingono sambamba na kuwashikilia utumwani, hivyo akasema..

(Sauti ya Zeid)

“Kushinda kitisho hiki dhidi ya amani, kutahitaji hatua endelevu ambazo ni zaidi ya matumizi ya nguvu za kijeshi.”

Pierre Buyoya mwakilishi maalum wa Muungano wa Afrika huko Mali na Sahel akazungumzia harakati dhidi ya Boko Haram wakati huu ambapo kikundi hicho kimeapa uaminifu kwa magaidi wa ISIL au Da’esh.

(Sauti ya Buyoya)

“Kuhusu suala mahsusi la jeshi la kimataifa dhidi ya Boko Haram, usaidizi wa fedha, kiufundi na vifaa kutoka Umoja wa Mataifa ni muhimu.”

Ombi la kufanyika kwa kikao hicho maalum kuhusu Boko Haram liliwasilishwa wiki iliyopita na Algeria kwa niaba ya kundi la Afrika kwenye Baraza la haki za binadamu.