Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 50 ya nchi duniani hazijatimiza uandikishwaji wa watoto shuleni

Asilimia 50 ya nchi duniani hazijatimiza uandikishwaji wa watoto shuleni

Tangu kuzinduliwa kwa malengo ya Elimu kwa wote miaka 15 iliyopita huko Dakar, nchini Senegal, ni asilimia 50 ya nchi zote duniani ambazo zimetimiza malengo hayo ya kuandikisha watoto wote shule ya msingi.

Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni UNESCO itakayochapishwa tarehe Tisa Aprili kabla ya kongamano la kimataifa la elimu litakalofanyika Korea Kusini mwezi Mei mwaka huu.

Ripoti hiyo iitwayo Elimu kwa wote 2000-2015; Mafanikio na changamoto, imesema pamoja na baadhi ya nchi kutimiza, ni theluthi moja tu ya nchi hizo zimeweza kufikia malengo yote Sita ya Elimu kwa wote ambayo yalipitishwa wakati wa kongamano la kwanza la elimu kwa wote huko Senegal.

Malengo hayo ni kuongeza huduma za elimu ya awali kwa watoto ikiwemo wale wenye ulemavu, kuhakikisha watoto wote wanahitimu elimu ya msingi, kuwapatia elimu vijana na watu wazima, kuongeza kwa asilimia 50 uwiano wa uwezo wa kusoma na kuandika baina ya wanawake na wanaume, kupunguza tofauti za kijinsia kwenye elimu ya msingi na sekondari na kuimarisha ubora wa elimu.

Ripoti hiyo itajadiliwa kwenye Kongamano la Korea Kusini.