Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa UM Lebanon azuru kambi ya Wapalestina Ein El-Hilweh

Mratibu wa UM Lebanon azuru kambi ya Wapalestina Ein El-Hilweh

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Sigrid Kaag amezuru leo kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Ein El-Hilweh kusini mwa Lebanon.

Akiwa ameandamana na Bi Heli Uusikyla, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakmibizi wa Palestina, UNRWA, Bi Kaag amekutana na wawakilishi wa kambi hiyo, ambao wamemweleza kuhusu hali ya kijamii, kiuchumi na usalama kwenye kambi hiyo.

Amesema wakati wa ziara yake, ameelezwa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo, zikiwemo msongamano wa watu kambini, ukosefu wa ajira na umaskini.

Aidha, Bi Kaag amezuru kituo kimoja cha afya kinachoendeshwa na UNRWA, pamoja na shule na kituo cha wanawake.