Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasyria hawaombi kuhurumiwa, wanaomba msaada- Ban

Wasyria hawaombi kuhurumiwa, wanaomba msaada- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameuambia mkutano wa kutoa ahadi za ufadhili kwa ajili ya Syria mjini Kuwait kuwa, watu wa Syria ni waathiriwa wa tatizo baya zaidi la kibinadamu la nyakati zetu, huku akikumbusha kuwa raia hao wa Syria hawaombi kuhurumiwa, bali wanaomba kusaidiwa.

Akielezea aliyojionea wakati alipozuru kambi za wakimbizi Uturuki, Jordan na Iraq, Ban amesema kuwa anaona aibu, kukasirishwa na kusikitishwa na kushindwa kwa jamii ya kimataifa kukomesha vita Syria. Ameongeza kwambaUstawi wa kikanda unavurugwa na mzigo wa mzozo wa Syria, huku takriban nusu ya watu wa Syria wakiwa wamelazimika kukimbia makwao.

"Tunawasilisha misaada ya kibinadamu ndani na nje mwa Syria lakini changamoto kubwa ni kuwafikia watu hawa. kwa hiyo kuna Takriban raia milioni 5 wa Syria wamenaswa katika maeneo ambayo yamezingirwa.Changamoto kubwa ambayo tunakabiliana na yo katika kuwasilisha misaada ya kibindamu ni kufikia watu hawa"

Kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu, Ban amesema ni lazima uhalifu mbaya usipite bila kuadhibiwa, kwani watu wa Syria wanahitaji uwajibikaji.

Kuhusu ufadhili wa misaada, Ban amesema mkutano wa mwaka uliopita ulipata ahadi za ufadhili wa hadi bilioni 2.4, lakini mahitaji bado yanazidi kuongezeka na ndiyo maana ombi la mwaka 2015 ni dola bilioni 8.4. Pamoja na misaada ya kunusuru maisha, ufadhili huu unaendeleza uthabiti ndani na nje ya Syria. Mkutano huu wa tatu Kuwait ni fursa ya jamii ya kimataifa kuonyesha ukarimu na kudhihirisha jinsi usaidizi wa kibinadamu na wa maendeleo unavyoweza kuunganishwa.

Aidha, Ban ameonya kuwa hakuna majibu rahisi kwa mzozo huo katili wa Syria, lakini akasema inajulikana dhahiri kuwa suluhu bora la kibinadamu kwa taabu ya watu wa Syria ni kumaliza vita kwa suluhu la kisiasa.