Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikwete aitaka jamii ya kimataifa isaidie Afrika kupambana na ukosefu wa ajira

Kikwete aitaka jamii ya kimataifa isaidie Afrika kupambana na ukosefu wa ajira

Wakati wa uzinduzi wa kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu ajira bora, linalofanyika kuanzia leo mjini New York, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema, ingawa amefurahi kuona kwamba ukosefu wa ajira umewekwa kipaumbele na jamii ya kimataifa hadi kuwa moja ya malengo ya maendeleo endelevu, bado nusu ya wafanyakazi duniani kote wanakumbwa na hali ngumu ya ajira, na wamekosa ruzuku ya serikali. Kwa kusikitishwa zaidi, amesema, ni kwamba tatizo hilo linakumba zaidi vijana na wanawake.

Akiongeza kwamba bado watu milioni 201 hawana kazi duniani, Rais Kikwete ameeleza kutiwa wasiwasi zaidi na hali iliyopo barani Afrika, ambapo idadi ya wanaoingia kwenye soko la kazi kila mwaka inazidi sana idadi ya ajira zinazozalishwa.

Aidha rais wa Tanzania amesema ni changamoto kwamba ukosefu wa ajira bora unaweza kuwa hatari kwa mshikamano wa jamii na hatimaye usalama wa nchi, huku akitaja vikundi vya kigaidi vinavyotumikisha vijana ambao hawana kazi.

Kwa mantiki hiyo, amesema ni muhimu kukuza mazingira yanayoweza kuvutia wawekezaji ambao wanazalisha ajira.

“ Nchi zinazoendelea zinapaswa kujitahidi kuweka sera kamili za uchumi pamoja na mifumo ya kuvutia uwekezaji. Nchi nyingi ikiwemo yangu, zimeshuhudia ufanisi katika ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha miongo miwili. Leo zaidi ya nchini 10 za kiafrika zinarekodi kiwango cha ukuaji wa uchumi cha takriban asilimia 5 hadi 6, ambacho ni kubwa zaidi kuliko kiwango cha ukuaji cha dunia kwa ujumla. Hii inafanya bara letu kuwa moja ya kanda zinazokua kwa kasi zaidi kiuchumi”

Hatimaye, rais Kikwete amezingatia tofauti kati ya nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea katika kutimiza malengo hayo, akisema nchi za kiafrika zinapaswa kusaidiwa:

“ Mawimbi ya watu wanojaribu kuingia Ulaya kwa boti hayatakoma iwapo umaskini na ukosefu wa ajira vitaendelea. Malisho yakiendelea kuwa kame kwa upande wa Afrika, na kunawiri kwa upande wa Ulaya, mtiririko hautasimama. Saidieni malisho ya  Afrika yanawiri."