Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mahitaji mapya ya kibinadamu kutokana na uchaguzi Nigeria- OCHA

Hakuna mahitaji mapya ya kibinadamu kutokana na uchaguzi Nigeria- OCHA

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya Kibinadamu, Kyung-wha Kang, amelihutubia Baraza la Usalama leo kuhusu mahitaji ya kibinadamu kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria na nchi jirani, akisema kuwa licha ya ripoti za mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na Boko Haram katika majimbo ya  Yobe, Gombe na Borno, hakuna mahitaji mapya yaliyoibuka kutokana na uchaguzi nchini humo.

Bi Kang amesema, zaidi ya raia 7,300 wameuawa na Boko Haram tangu mwanzoni mwa 2014 katika majimbo hayo matatu yaliyoko katika hali ya dharura, wakiwemo watu 1,000 mwaka huu pekee. Amesema shule na huduma za afya zimevurugika vibaya mno, na kuna ripoti za mara kwa mara za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ukiwemo ukatili wa kingono na kijinsia, na usafirishaji haramu wa watoto. Kuhusu usaidi wa kibinadamu, amesema

"Kuongezeka kwa vitendo vya kikatili vya Boko Haram kunaendelea kuzuia kuwafikia watu wanaohitaji usaidizi wa kibinadamu kwa dharura, na kubana uwezo wa juhudi zetu.Watu wapatao milioni 3 hawataweza kukimu mahitaji yao ya msingi ya chakula baada ya Julai mwaka huu wa 2015 bila usaidizi wa kibinadamu."

Amesema licha ya juhudi za serikali kuu na serikali za majimbo, juhudi za kibinadamu ni duni na hazijaratibiwa ipasavyo.

Hali ya kibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria bado ni mbaya mno, na kwamba mzozo huo unaendelea kuathiri vibaya wanawake, watoto na vijana, na wengine wengi ambao wameathiriwa na machafuko. Ufadhili wa ziada wa kuwezesha kukabiliana na mahitaji makubwa ya waathiriwa wa mzozo, unahitajika kwa dharura.”