Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili unaofanywa na Boko Haram umekithiri dunia isikae kimya:Chambas

Ukatili unaofanywa na Boko Haram umekithiri dunia isikae kimya:Chambas

Ukatili unaotekelezwa na kundi la kigaidi la Boko Haram umekithiri na kuvuka mipaka na hivyo kuwa tishio la dunia amesema mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu waUmoja wa Mataifa,  Magharibi mwa Afrika Mohammed Ibn Chambas.

Taarifa kamili na Amina Hassan

(TAARIFA YA AMINA)

Akihutubia  Baraza la Usalama kwa njia ya video katika kikao kilichojadili athari za vitendo haramu vinavyofanywa na kundi hilo la kigaidi Kaskazini mwa Nigeria na ukanda wa Afrika Magharibi, Bwana Chambas amesema Boko Haram wanaendelea kushambulia na kupora raia na hivyo kuathiri ustawi wa jamii hususani Kaskazini mwa taifa hilo.

Amesema watoto wameendeela kutumiwa kama silaha, kujumuishwa katika mapigano pamoja na kuuliwa huku shule nyingi zikifungwa kwa hofu ya mashambulizi na akashauri

(SAUTI CHAMBAS)

"Napenda kusisitiza kwamba njia ya kijeshi pekee haitatosha kuondoa tishio la Boko Haram. Jumuiya ya kimataifa inaweza na inapaswa kutimiza jukumu muhimu katika kusaidia ukanda  husika katika kutatua changamoto za kiuchumi, kijamii na kisisasa zinazohusihwa na Boko Haram."

Kwa upande wake msaidizi wa Katibu Mkuu na Naibu wa Mratibu wa Misaada ya Dharura, Kyung-wha Kang amesema misaaada ya kibinadmau inahitajika nchini humo na nchi jirani ambazo zimeshambuliwa na kundi hilo akitolea mfano wa watu zaidi ya laki mbili wanoahitaji misaada ya dharura nchini Cameroon na Chad baada ya kuwa wakimbizi wa ndani.