Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wamulika umuhimu wa maji kwa uhai

Umoja wa Mataifa wamulika umuhimu wa maji kwa uhai

Mwaka huu wa 2015, Umoja wa Mataifa ukitimiza muongo maalum wa kuchukua hatua kwa ajili ya maji kwa uhai, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala maalum ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Akizungumza wakati wa mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika leo mjini New York, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amekaribisha hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, akieleza kwamba watu bilioni 2 wamepata huduma za kujisafi na lengo la maendeleo ya milenia huhusu maji safi limetimizwa mwaka 2010 kabla ya ukomo wake.

Hata hivyo, Bwana Eliasson amesikitishwa na mabilioni ya watu ambao bado wanakosa huduma za kujisafi na za maji safi duniani kote, akiongeza kwamba mwelekeo ni kuongezeka kwa ukosefu huo kutokanana na mabadiliko ya tabianchi, na watu kuhamia mijini kwa wingi.

Aidha amelaani mkakati mpya wa waasi kadhaa kama Daesh wa kutumia maji kama silaha ya vita.

(Sauti ya Jan Eliasson)

“ Jamii zikikosa huduma za maji, mvutano unaongezeka. Inatia wasiwasi zaidi wakati wapiganaji wanazuia upatikanaji wa maji makusudi kama silaha ya vita. Inanifanya kukariri umuhimu wa kufanya maji yawe msingi wa ushirikiano. Vyanzo vya pamoja vya maji vimezileta nchi pamoja zaidi, katika historia. Kuliko kuona matumizi ya maji kwa pamoja kama shida, tunapaswa kuyaona kama suluhu, kupitia diplomasia bunifu na yenye nguvu”