Ban aelekea Kuwait kwa kongamano la ufadhili kwa Syria

30 Machi 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, leo anaugana na viongozi wengine nchini Kuwait kwa ajili ya kongamano la kimataifa la kutoa ahadi za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Syria hapo kesho. Akiwahutubia waandishi wa habari mjini Baghdad kabla ya kuelekea Kuwait, Ban amesema..

“Kutoka hapa, naelekea Kuwait kushiriki kongamano la kutoa ahadi za kuisaidia wakimbizi wa Syria na nchi jirani zinazowapa hifafhi. Ningependa kuipongeza serikali na watu wa Iraq kwa kuwapa kimbilio na usaidizi raia wengi wa Syria wanaokimbia mapigano.”

Wakati huo huo, Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, limesema takriban dola milioni 121 zinahitajika ili kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama wa chakula na kusambaratika kwa mifumo ya kuzalisha na kuuza chakula nchini Syria.

Mzozo wa Syria umevuruga uzalishaji wa kilimo na biashara, na kuwaacha watu wapatao milioni 9.8 bila usalama wa chakula.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Ertharin Cousin, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa isiwaache watu wa Syria.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter