Bado nahofia tatizo la usalama na athari kwa raia wa Iraq- Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-moon, amesema kuwa bado anatiwa wasiwasi na tatizo la kiusalama nchini Iraq na athari zake kwa raia.
Ban amesema hayo akikutana na wanahabari mjini Baghdad, mara tu baada ya kukutana na Waziri Mkuu, Haider al-Abadi, Rais Fuad Masum na Spika wa Bunge Saleem al-Jabouri.
Ban amesema, wametathmini hatua zilizopigwa kaika operesheni za kuyakomboa maeneo yanayodhibitiwa na Daesh, yakiwemo yale yaliyoko karibu na Tikrit.
“Natumai kuwa maeneo mengine na ukanda mzima utakombolewa kutokana na tishio la Daesh. Watu wameathiriwa kwa kiwango kikubwa kutokana na wimbi hii jipya la machafuko, ukiwemo ukatili wa kingono na wa kijinsia. Zaidi ya watu milioni 2.5 wamelazimika kuhama makwao. Jamii za walio wachache, wanawake na watito ndio wanaoathiriwa hasa zaidi.”
Ban amesema kuwa vitendo vya Daesh vimelenga pia urithi wa kitamaduni wa Iraq.
“Nalaani vikali uharibifu wa maeneo ya kihistoria Hatra, Nimrud na kwingineko, na naelezea kuunga mkono juhudi za UNESCO kulinda maeneo ya utamaduni yaliyoko hatarini. Ni lazima tuungane kulinda urithi wa pamoja wa ubinadamu.”
Katibu Mkuu amesema, serikali ya Iraq imejitahidi kuwasaidia walioathirika na machafuko, lakini bado kuna changamoto kubwa, na ufadhili zaidi wahitajika ili kunusuru maisha, pamoja na kuwalinda raia kutokana na ukatili.