Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya saa ya moja kwa ajili ya dunia yamulika mabadiliko ya hali ya hewa

Kampeni ya saa ya moja kwa ajili ya dunia yamulika mabadiliko ya hali ya hewa

Taa za majengo ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa zitazimwa leo usiku pamoja na zaidi ya majengo maarufu 1,200 duniani kote, viwanda, nyumba za watu binafsi, ofisi, ili kuonyesha mshikamano wa kimataifa katika kupambana na madabiliko ya tabianchi.

Kampeni hiyo iitwayo ¨Earth Hour¨ yaani saa moja kwa ajili ya dunia, imeanzishwa mwaka 2007 na Mfuko wa Kimataifa wa wanyama pori, WWF ikifuatiliwa na mamilioni ya watu duniani.

Katika ujumbe wake kwa ajili ya siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mabadiliko ya hali ya hewa ni shida kwa watu, yanawaathiri, lakini pia watu wakiungana wanaweza kukabiliana nayo. Aidha amesema kwamba kampeni hiyo ni njia ya kumulika mahitaji ya watu bilioni moja ambao bado hawapati huduma za umeme duniani kote.

Miongoni mwa majengo yatakayozimwa leo ni Eiffel Tower ya Ufaransa na Golden Gate ya San Francisco, Marekani. Kenya na Uganda zitashiriki pia kwenye maadhimisho ya siku hii.