Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa inapaswa kuonyesha nguvu zake dhidi ya ugaidi

Jamii ya kimataifa inapaswa kuonyesha nguvu zake dhidi ya ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema raia wa kawaida wanajiuliza kwa nini nchi zinazojiita “Umoja wa Mataifa” hazijaweza kupambana na hatari ya ugaidi na kuiondoa. Ameongeza kwamba kinachoendelea mashariki ya kati ni mpango wa kikatili wa kuwaangamiza watu kwa msingi wa kidini au kikabila.

Amesema hayo akizungumza wakati wa mjadala wa wazi kuhusu wahanga wa mashambulizi na ukiukwaji dhidi ya makundi ya walio wachache Mashariki ya Kati, uliofanyika leo katika Baraza la Usalama.

Amesema watu hao, wakiwemo Wakristo, Wayazidi, Wakurdi hawana la kufanya isipokuwa kukimbia, kusilimu au kufa.

“ Hatari ni kuangamia kabisa kwa makundi ya walio wachache. Jamii ya kimataifa haipaswi kuacha kitu kama hicho kitokee. Sisi ni jamii ya kimataifa; hatupaswi tena kuwa mamlaka bila nguvu”.

Aidha ameeleza kwamba usaidizi wa kibinadamu hautoshi ili kuokoa watu hao, akisema ni lazima kuonyesha ujumbe wa aina mbili:

“ Mshikamano na wanaoteswa na ukali dhidi ya magaidi. Kwa makundi ya walio wachache Mashariki ya Kati, tunapaswa kuonyesha kwamba tuko upande wao, na kwa upande wa serikali zinazoheshimu tofauti za makundi. Kwa magaidi wa Daesh, tunapaswa kuwaonyesha kwamba tutapigana nao bila kusimama hadi kuwaondoa”

Miongoni mwa hatua ammbazo amependekeza zichukuliwe na jamii ya kimataifa ni Mfuko maalum wa kurejesha wakimbizi makwao na kuwajengea upya nyumba na makanisa, kuongeza nguvu za kijeshi ili kuhakikisha uwepo wa usalama katika maeneo yatakayoachiliwa na Daesh, na suluhu la kisiasa ili kujengea uwezo wa serikali zinazoshuhudia matatizo hayo.

Hatimaye, amekariri umuhimu wa kupambana na ukwepaji wa sheria kwa watekelezaji wa uhalifu wa kivita, akiziomba nchi za ukanda huo kusaini mktaba wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.