Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lizipeleke kesi za Iraq na Syria ICC- Kamishna Zeid

Baraza la Usalama lizipeleke kesi za Iraq na Syria ICC- Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, amelitaka Baraza la Usalama la Umoja huo lichukuwe hatua mathubuti ili kuikomesha mizozo ya Iraq na Syria kwa kuzipeleka kesi za mizozo hiyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC.

Kamishna Zeid amesema hayo akilihutubia Baraza hilo kwa njia ya video kutoka Geneva, wakati likifanya mjadala wa wazi kuhusu wahanga wa mashambulizi na ukiukwaji dhidi ya makundi ya walio wachache kikabila au kidini Mashariki ya Kati.

Kamishna Zeid amesema jamii ya kimataifa huzingatia haki za walio wachache kwa njia ya upendeleo na isiyo ya kina, kwani serikali humulika tu jamii ambazo zinahusiana nazo kitamaduni, na haki za jamii za walio wachache huangaziwa tu pale kunapoibuka ukatili uliokithiri.

“Iwapo tutajali tu haki za walio wachache baada ya wao kuanza kuchinjwa, basi hapo tukakuwa tayari tumeshindwa. Itikadi kali hunawiri pale kutovumiliana na viwango vya haki za binadamu tayari ni hafifu. Hunawiri katika nchi zinazowasaliti watu wao, zinazoshindwa kulinda katiba zao, na ambazo hazizingatii utofauti wa wa jamii zao kikabila, kilugha na kidini.”

Aidha, Kamishna Zeid amelitaka Baraza hilo kuchukua hatua za kuimaliza mizozo ya Yemen, Libya na nchi nyingine, akihoji umuhimu wa kutochukua hatua au kuchelewa kuchukua hatua kama hizo.

“Au tunataka tusubiri hadi uwezo wa waathiriwa, na wa ubinadamu wote kutoa machozi zaidi uishe, na mawe pekee ndiyo yasalie na uwezo wa kulia? Na ni lipi zuri litatokana na hilo? Ni lipi litakalokuwa zuri kwetu sote, iwapo hatua kamwe haiwezi kuchukuliwa, au ichukuliwe ikiwa imekawia sana, na hivyo kutokuwa na maana yoyote?”