Skip to main content

Hali ya kibinadamu Syria imezorota, yataka suluhu la kisiasa

Hali ya kibinadamu Syria imezorota, yataka suluhu la kisiasa

Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, jamii ya kimataifa inapswa kuonyesha ari zaidi ili kufikia suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Syria.

Bi Amos amesema, kama baraza hilo lilivyosema mara kwa mara, hakuna suluhu la kibinadamu kwa mzozo huo, ambao sasa umeingia mwaka wa tano, huku ukifikia viwango vya kutisha vya ukatili, licha ya baraza hilo kupitisha azimio namba 2139. Azimio hilo lilizitaka pande zinazozozana kuchukua hatua za kukomesha mashambulizi dhidi ya raia na kuwezesha wahudumu wa kibinadamu kuwafikia wale wenye mahitaji.

Amesema wote walitarajia kuwa azimio hilo lingezilazimu pande zinazozozana kupunguza machafuko na kuchangia kuboresha hali ya watu wa Syria, lakini badala yake, hali imezorota hata zaidi. Bi Amos amewahutubia waandishi wa habari, mara tu baada ya kulihutubia Baraza la Usalama

“Nimewakumbusha wajumbe wa baraza hilo ni raia ndio wanaoendelea kuathirika zaidi na mzozo huo. Katika siku chache zilizopita pekee, tumesikia kuhusu kuongezeka kwa machafuko Idlib, na kukazwa kwa kizuizi kwa mamia ya maelfu ya watu walionaswa katika mji huo. Watoto wanaendelea kuathiriwa vibaya mno, na takriban thuluthi tatu ya watu wa Syria wanakadiriwa kuishi katika umaskini uliokithiri.”