Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko India kwa usaidizi wa kudhibiti saratani: IAEA

Heko India kwa usaidizi wa kudhibiti saratani: IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA, Yukia Amano amesema kuanzishwa kwa mipango bora ya kudhibiti saratani kwenye nchi zinazoendelea kunadhihirisha jinsi teknolojia ya nyuklia inavyoweza kuchangia maendeleo duniani.

Bwana Amano amesema hayo wakati wa ziara yake kwenye kituo cha saratani cha hospitali ya kumbukumbu ya Tata mjini Mumbai, nchini India.

Amesema ugonjwa wa saratani sasa ni tishio la afya kwa nchi zinazoendelea lakini idadi kubwa ya nchi hizo hazina rasilimali za kukabiliana nao.

Bwana Amano amesema kitendo cha kuwa na vituo na vifaa vya kudhibiti saratani au hata kutibu kinaweza kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa.

Kwa mantiki hiyo ameisifu India kwa msaada wake katika jitihada za kimataifa za kudhibiti saratani akitolea mfano mashine za tiba ya minunurisho zinazotolewa na nchi hiyo kwa nchi zinazoendelea halikadhalika wataalamu.

IAEA inasema ifikapo mwaka 2020 zaidi ya watu Milioni 10 watakuwa wanafariki dunia kila mwaka duniani kote na idadi kubwa ikiwa ni katika nchi za vipato vya chini na kati.