Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuyakalia maeneo ya Wapalestina na mizozo inaongeza mahitaji ya kibinadamu- OCHA

Kuyakalia maeneo ya Wapalestina na mizozo inaongeza mahitaji ya kibinadamu- OCHA

Mahitaji ya kibinadamu katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa yanaongezekakutokana na kuendelea kwa Israel kuyakalia maeneo hayo na mizozo ya mara kwa mara, kulingana na tathmini ya mwaka 2014 ya Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA.

Kulingana na ripoti hiyo iitwayo, “Maisha yaliyovurugika”, raia wa Palestina wanaendelea kuwa wahanga wa vitisho kwa maisha yao, usalama wa kimwili na uhuru wao.

Ripoti hiyo imesema mwaka 2014 ulishuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia tangu mwaka 1967.

Ramesh Rajasingham, ni Mkuu wa OCHA katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa..

“Mwaka 2014 ulikuwa wa kusikitisha Gaza. Tayari, tangu mwaka 2007 walikuwa wameshuhudia vikwazo vya kutembea barabarani, baharini na hata angani, wakipata ugumu kutembea, kuuza bidhaa nje au kuzinunua, na kuishi maisha ya kawaida, hasa kwa sababu ya vizuizi vilivyowekwa na serikali ya Israel kufuatia kuchukuliwa kwa Ukanda wa Gaza na Hamas.”

Amesema, hali ya uchumi na kibinadamu ambayo tayari ilikuwa imedhoofika Gaza, ilifanywa kuzorota hata zaidi kufuatia mzozo wa Julai na Agosti mwaka uliopita, ambako zaidi ya raia 1,500 waliuawa, wakiwemo watoto 500.

Hapa tena ni Ramesh Rajasingham..

“Na miongoni mwa watu 10,000 waliojeruhiwa Gaza, 3,000 walikuwa watoto. Na kati ya watoto hao 3,000, 1,000 wanakabiliwa na athari za kudumu za majeraha waliyopata. Kwa hiyo, si tu idadi ya wahanga, lakini pia madhara watakayokabiliana nayo baadhi ya watoto katika maisha yao yote kimwili.”