Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ana taarifa za kinachoendelea Yemen

Ban ana taarifa za kinachoendelea Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ana taarifa ya kwamba Saudi Arabia imetangaza kuanza operesheni za kijeshi nchini Yemen kufuatia ombi la serikali hiyo.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari akiseam kuwa Ban ana taarifa kuwa nchi nyingine hususan zile ambazo ni wanachama wa baraza la ushirikiano wa ghuba, CGG zinaunga mkono operesheni hizo.

“Katibu Mkuu akirejelea taarifa ya Rais wa baraza la usalama ya tarehe 22 Machi ambayo huku ikiunga mkono uhalali wa Rais wa Yemen, Abdo Rabbo Mansour Hadi, inatoa ametoa wito kwa pande husika nchini Yemen na nchi wanachama kujizuia kuchukua hatua yoyote inayoweza kudidimiza umoja, mamlaka na uhuru wa Yemen. Baraza la usalama pia linatoa wito kwa nchi wanachama kujizuia kuingilia mambo ya ndani kwani kitendo hicho kinaweza kuibua mzozo na ukosefu wa utulivu na badala yake limetaka usaidizi wa mpito wa kisiasa.”

Halikadhalika Katibu Mkuu ametaka pande zote husika kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa ili kuhakikisha raia wanalindwa, halikadhalika wafanyakazi wa misaada bila kusahau sheria zinazolinda haki za binadamu na wakimbizi.

Ban pia ameunga mkono hatua za mjumbe wake maalum Yemen akisema ataendelea kufuatilia kwa karibu hali inavyoendelea nchini humo.