Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataja changamoto za mkataba wa kupinga matumizi ya silaha za kemikali:

Ban ataja changamoto za mkataba wa kupinga matumizi ya silaha za kemikali:

Miaka 40 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za kikemikali, kuna matumaini kwasababu katika kipindi hicho kumekuwepo na jitihada za pamoja za kutokomeza matumizi yake.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa siku ya leo ya mkataba huo wa kupinga matumizi ya silaha za kemikali duniani unaojumuisha pia zile za kibaiolojia.

Ban amesema licha ya matumaini, ni lazima kuendeleza kuwa macho kwani ripoti za wataalamu zinaonyesha kuwa usimamizi wa mkataba huo unakabiliwa na changamoto kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia halikadhalika vitendo vya magaidi na vikundi visivyo vya kiserikali.

Ametolea mfano mlipuko  wa Ebola huko Afrika Magharibi akisema umedhihirisha hasara inayoweza kusababishwa na magonjwa na athari mbaya zaidi iwapo magonjwa yanaweza kutumiwa kama silaha.

Hata hivyo amesema vile ambavyo jamii ya kimataifa ilishiriki kukabiliana nao ni ishara ya jinsi jamii hiyo inaweza kukabiliana na vitisho iwe vya kiasili au vya kupangwa.

Kwa mantiki hiyo ametaka nchi zitumie siku hii kukataa kwa kauli moja matumizi ya magonjwa kama silaha huku akizisihi nchi 23 ambazo  bado hazijatia saini mkataba huo kufanya hivyo kwa kuwa hadi sasa ni nchi 173 pekee zinazouunga mkono.