Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakhbali wa afya CAR uko njiapanda:WHO

Mustakhbali wa afya CAR uko njiapanda:WHO

Shirika la afya duniani, WHO na wadau wake wanahitaji dola Milioni 63 kwa ajili ya huduma za tiba na afya ya uzazi huko Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR.

WHO imesema kiasi hiyo kinalenga kuimarisha huduma za afya ambazo bado hazijakwamuka licha ya amani kuimarika kwa kiasi fulani.

Kwa mujibu wa WHO, nchini CAR vituo vya kutoa huduma za afya ambavyo vinafanya kazi ni asilimia 55 tu na karibu vyote vinategemea msaada kutoka mashirika ya kiraia na yale ya Umoja wa Mataifa.

Mwaka 2014 wadau wa afya yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa yalitoa vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa 800,000 huku wakitoa huduma kwa watu wengine zaidi ya 600,000 nchini humo.

WHO inasema bila ufadhili wa fedha, huduma za afya nchini CAR zitasitishwa kwa kuwa mwelekeo wa kuimarika kwa huduma za afya uko mashakani wakati huu uchaguzi unakaribia na kuna uwezekano wa mlipuko wa magonjwa na ghasia.