Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya waomba hifadhi ilivunja rekodi mwaka 2014 - UNHCR

Idadi ya waomba hifadhi ilivunja rekodi mwaka 2014 - UNHCR

Vita nchini Syria na Iraq, pamoja na mizozo ya silaha katika nchi zingine, vilisababisha kuongezeka kwa idadi ya waomba hifadhi katika nchi zilizostawi kwa kiwango kikubwa zaidi katika kipindi cha miaka 22. Taarifa kamili na Joseph Msami.

Taarifa ya Msami

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, kuhusu mwelekeo wa uombaji hifadhi mwaka 2014, ambayo imesema uombaji hifadhi mwaka huo ulivunja rekodi ya miaka 22.

Idadi ya watu waliofanya maombi ya hifadhi mwaka 2014 ilifikia 866,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45 kutoka ile ya mwaka 2013, ambako ni watu 596,000 walioomba hifadhi. Iraq na Syria zilichangia pakubwa idadi hiyo, lakini pia nchi za Afrika kama Eritrea, Nigeria, Gambia na Mali zimetajwa kuchangia mwelekeo huo. Melissa Flemming ni msemaji wa UNHCR

Migogoro mingine ya silaha, ukiukwaji wa haki za binadamu, na pia kuzorota kwa hali ya usalama na hali ya kibinadamu katika nchi jirani, kumeisukuma idadi ya waomba hifadhi katika nchi zilizostawi kiviwanda kufikia idadi ya juu zaidi katika miaka 22, mwaka uliopita. Kile tulichoshuhudia pia ni kwamba raia wa Syria ndio waliokuwa wengi zaidi, wakichangia takriban maombi 150,000.”

Idadi ya mwaka 2014 ndiyo ya juu zaidi tangu mwaka 1992, ulipoanza mzozo wa Bosnia na Herzegovina.