Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima wanawake tukaze mwendo safari ndefu: Rais Ellen Jonhson Sirlief

Lazima wanawake tukaze mwendo safari ndefu: Rais Ellen Jonhson Sirlief

Bado nafasi ya mwanamke ni finyu duniani kwa mfano malipo ya mishahara kwa wanawake yanatofautiana na wanaume kwasababau tu za kijinsia. Ni sehemu ya kauli ya Rais wa Liberia Ellen Johnson-Sirleaf wakati akihojiwa na Joseph Msami wa Idhaa hii jijini New York, Marekani. Rais huyo wa kwanza mwanamke barani Afrika pia amesema ili kuepuka migogoro Afrika ni lazima kupatia suluhu la vyanzo vya migogoro. Hapa anaanza kwa kujibu swali je anajisikiaje kuwa Mwanamke wa kwanza Rais wa kuchaguliwa barani Afrika?

Rais Ellen Johnson Sirleaf: Mtu ni lazima afurahishwe na hilo. Kuweza kuvunja ukuta huo ambao umekuwa thabiti mno kwa miaka 50 iliyopita. Lakini pia, unapaswa kunyenyekea, kutokana na wajibu ambao wadhfa huo unabeba, kwani unawakilisha matarajio na ndoto za wanawake, si tu Afrika,  bali kote duniani. Kwa hiyo, ni hisia nzuri, lakini pia ni hisia za unyenyekevu, kutokana na ukubwa wa wajibu huo.

Swali: Na kutokana na kwamba ni wewe pekee ambaye umechaguliwa na watu, je unahisi mzigo mkubwa?

Rais Ellen Johnson Sirleaf: La hasha! Mara kwa mara huwaambia watu kuwa mie ni mtaalam. Nimekuwa katika nafasi za uongozi katika njia nyingi- kimataifa, na pia kitaifa. Kwa hiyo, imenipeleka tu kwa daraja ya juu Zaidi, na wajibu mkubwa Zaidi, lakini nahisi kuwa namudu vyema katika wadhfa huo.

Swali: Huu ni mwaka wa 20 tangu kuanzishwa kwa jukwaa la Beijing lililotaka usawa wa kijinsia, kuna mabadiliko yoyote hususani barani Afrika?

Rais Ellen Johnson Sirleaf : Oh bila shaka! Hii leo tuna watoto wengi wa kike shuleni, tuna wanawake ambao ni mawaziri, idadi ya wanawake bungeni imeongezeka kwenye nchi nyingi. Chukua tu mfano wa Rwanda! Rwanda ina idadi kubwa ya wanawake wabunge duniani, na siyo tu Afrika. Tuna wanawake wengi mawaziri, wanawake wanaoshika nafasi za utendaji. Wanawake wengi zaidi wanaofungua biashara zao. Hebu fikiria wanawake wa kijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wa pembezoni. Hii leo wana sauti, na nikitembelea vijijini wananiambia, Mheshimiwa Rais leo tunaweza kuketi kwenye mkutano, kuzungumza tunaweza kueleza mambo yetu na tunaweza kushiriki. Hata kama watu hawakubali lakini tunaweza kusema. Nadhani hayo ni mafanikio makubwa na tuseme kwamba miaka 20 baada ya Beijing. Kuna mafanikio lakini bado kuna pengo kubwa. Bado idadi ya wanawake viongozi wan chi ni ndogo, bado kuna wasichana ambao hawamalizi shule. Kuna wanawake wa vijiji ambao licha ya kupata sauti bado hawana uwezo wa kupata nyezo za uzalishaji mfano mikopo, ardhi na wakati mwingine ufahamu.  Na kwenye sekta binafsi bado hatuna wa kutosha mfano maafisa watendaji wakuu. Na baadhi ya nchi haziwapatii wanawake fursa sawa. Hawako bungeni, nafasi za utendaji, serikalini. Kimataifa kuna baadhi ya wanawake ambao wanaongoza mashirika ya Umoja wa Mataifa, hususan wawakilishi wa Katibu Mkuu lakini bado wako kundi la wachache. Na bado leo hii wanawake wanapata ujira pungufu kuliko mwanaume licha ya kufanya kazi sawa. Tuna safari ndefu.

Swali: Hebu tuzungumzie sasa ulinzi wa amani na usalama ambalo ni moja ya jukumu kuu la Umoja wa Mataifa, unadhani dunia ifanye nini ili kuzuia migogoro hususani barani Afrika ambapo imesababisha kudorora kwa maendeleo ya kiuchumina kijamii?

Rais Ellen Johnson Sirleaf :Kwa kawaida nasema kwamba kinga ni bora kuliko tiba hususan kuhusu mizozo, nadhani inabidi kutarajia na kuona viashiria mapema wakatia tunaona uhasama ukizuka katika jamii wakati tunaona ishara ya kukandamizwa kwa watu.Tujiulize ni nini tunaweza kufanya haraka ili kuweza kusaidi mataifa hayo ili yaweze kuweka taasisi ambazo zitaweza kukabiliana na matarajio na  uhasama kabala hujawa mzozo. Hilo najua ni jambo ambalo kila mtu analiwazia na ni jambo ngumu kwa sababu huwezi jua ni lini mzozo utaibuka lakini kuna viashiria. Sitataja nchi yeyeote lakini ukweli ni kwamba ukiangalia baadhi ya nchi unaona uhasama unaendelea na sasa ndio wakati wa kutuma ujumbe wa amani kwenda kutafiti uwezekano wa kuzuka kwa mzozo na mikakati inayoweza kuwekwa kumaliza au kpunguza. Nadhani hilo ndilo suluhu kwa sababu wakati mzozo unapozuka gharama ni kubwa  kwa ajili ya nchi na pia katika raslimali za kukabiliano na mzozo.