Skip to main content

Nimeibiwa utoto wangu, asema kijana aliyetumikishwa vitani DRC

Nimeibiwa utoto wangu, asema kijana aliyetumikishwa vitani DRC

Huyu ni Junior Nzita Nsuami, kijana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC aliyeetumikishwa na waasi wakati wa vita dhidi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko. Anasema amepitia mateso mengi mwilini mwake, yeye ni mhanga wa utumikishwaji watoto vitani na ametumikishwa na waasi wakati akiwa na umri wa miaka 12.

Junior ametoa simulizi hiyo alipohutubia mjadala maalum wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akiwa sasa ni Balozi mwema kuhusu kampeni ya Umoja huo “Watoto si jeshi” nchini DRC.

Ameeleza kwamba waasi waliwalazimisha yeye na marafiki zake kuungana nao wakiwa shuleni, akilazimishwa kupigana nao kwa kipindi cha miaka 10.

“ Tumeiba, tumeua, Tumefanya vyote tulivyoambiwa tukikiuka haki za kimataifa ya kibinadamu. Niruhusiwe kuomba msamaha tena kwa mabaya yote niliyofanya na wenzangu. Mpaka sasa hivi najuta”

Junior akaongeza kwamba utaratibu wa kujisalimisha na kurejea kwenye jamii umemsaidia kuendelea na masomo na kujijenga.

Hivi sasa, anaongoza shirika lisilo la serikali “ Paix pour l’Enfance”, yaani amani kwa utoto, akisema anajituma ili kujenga mustakhabali bora kwa watoto wanaopitia mateso kama yale aliyoyapitia.

Wakati huo huo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, umetangaza leo katika mkutano wa wiki wa uandishi wa habari kwamba tayari zaidi ya watoto 500 waliokuwa wametumikishwa vitani wameachiliwa na waasi wa FDLR, FRPI na ADF tangu mwanzo wa mwaka.

Aidha jeshi la kitaifa nchini humo, FARDC limeiruhusu MONUSCO kutathmini wanajeshi wake mashariki mwa DRC, MONUSCO ikithibitisha kwamba hakukuwepo mtoto hata mmoja miongoni mwao.