Skip to main content

Ukiukwaji wa haki unaotisha umefanyika Iraq- Ripoti

Ukiukwaji wa haki unaotisha umefanyika Iraq- Ripoti

Ukiukwaji wa haki za binadamu ambao watu wa Iraq wamekuwa wakikumbana nao ni mkubwa na ulioenea kwa njia inayotisha. Hayo yamesemwa na Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Flavia Pansieri.

Bi Pansieri amesema hayo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu, akiwasilisha ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iraq katika muktadha wa ukiukwaji uliotendwa na kundi linalojiita ISIL, linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, likishirikiana na makundi mengine.

“ISIL, ni dhahiri kuwa inalenga kusambaratisha utofauti wa kabila na dini ulioshamiri Iraq, na imetekeleza uhalifu wa kutisha dhidi ya Wakristo, Wakaka’e, Wakurdi, Wasabea-Mandea, Washi’a, Waturki, na Wayazidi, siyo kwa sababu nyingine, ila imani zao za kidini au asili yao.”

Bi Pansieri amesema taarifa zilizokusanywa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, zinaonyesha kuwa kumekuwepo vitendo vya uhalifu wa dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na ukiukwaji mwingine mbaya zaidi wa haki za binadamu, hususan dhidi ya wanawake na wasichana, pamoja na kuwafanya watu watumwa, uuzaji wa wanawake na wasichana, ubakaji, kulazimisha watu kuhama, na vitendo vingine vya kinyama na vya kudhalilisha.

“Taarifa zilizokusanywa na ujumbe huo inaonyesha kuwa ISIL huenda wametekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wayazidi, wakifanya mauaji ya kupangwa, kusababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili, na kuhamisha watoto kwa lazima, kwa lengo la kuwaangamiza Wayazidi kama kundi.”

Ripoti hiyo imetaja pia ukiukwaji uliotekelezwa na vikosi vya usalama vya Iraq na wanamgambo wanaohusiana navyo, ukiwemo utesaji na mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia. Baraza la Haki za Binadamu limeitaka serikali ya Iraq ifanye kila iwezalo kuwalinda raia, na kuwataka wanaoutekeleza uhalifu dhidi ya raia kufikishwa mbele ya sheria.