Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM hautabagua wanandoa wa jinsia moja

UM hautabagua wanandoa wa jinsia moja

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya usimamizi katika Umoja wa Mataifa, Yukio Takasu, amesema leo kuwa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu ikielekeza kuhusu marupurupu ya wafanyakazi wa Umoja wa huo ikiwemo pale wanapofunga ndoa, ilitokana na kanuni za Umoja wa Mataifa za utangamano wa watu wenye asili tofauti na kutobagua.

Bwana Takasu amesema hayo wakati Kamati ya Tano ya Umoja wa Mataifa ikikutana kupiga kura kuhusu rasimu ya azimio lililowasilishwa na Urusi, likitaka taarifa hiyo ya Katibu Mkuu itupiliwe mbali kwa misingi kuwa hakuomba ushauri wa nchi wanachamam, na kwamba kuitekeleza hatua hiyo kungeongeza gharama ya matumizi kwa Umoja wa Mataifa.

Taarida ya Katibu Mkuu iliamrisha kulipa marupurupu kwa wafanyakazi ambao ndoa zao au watoto wao wanatambuliwa kisheria pale wanapofungia ndoa au kuhalalisha uzazi wao, bila kubaguliwa kwa misingi ya jinsia ya watu wanaofunga ndoa nao.

Bwana Takasu amesema uamuzi wa Katibu Mkuu ulitokana na kuzingatia kwa makini na kutambua dhana tofauti za nchi wanachama kuhusu suala hili, na unaoana kikamilifu na maazimio ya Baraza Kuu.

“Baraza Kuu linatambua kanuni za utofauti wa watu wanaohudumu katika shirika hili. Kwa kuwa Katibu Mkuu na wafanyakazi wanapigia debe maadili na kanuni za kutobagua, tunatumai kuwa Baraza Kuu litatambua mamlaka ya Afisa Msimamizi ya kufanya uamuzi kuhusu masuala ya usimamizi, ambao unauiana na maadili yetu na wajibu wetu kisheria. Katibu Mkuu anaamini uungaji mkono wenu kuwa hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa tunakofanyia kazi. Umoja wa Mataifa ni lazima uongoze kwa mfano.”

Rasimu ya azimio la Urusi imepingwa na nchi wanachama, ikiungwa mkono kwa kura 43 pekee. Nchi 80 zimeipinga rasimu hiyo, huku nchi 37 zikionyesha kutoegemea upande wowote.