Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waendelea kuathirika zaidi na mzozo Yemen

Watoto waendelea kuathirika zaidi na mzozo Yemen

Vurugu inayoendelea nchini Yemen inazidi kuathiri watoto, idadi ya watoto wanaouawa au kujeruhiwa mwaka 2014 ikiwa imeongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 2013.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Christophe Boulierac, amesema hali hiyo imesababishwa na mapigano yanayozidi nchini humo, akitaja mfano wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea kwenye misikiti ya mji mkuu Sanaa, wakati wa sala ya Ijumaa, tarehe 20 Machi, ambapo watoto 12 wamepoteza maisha na wengine 20 kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, msemaji huyo amesema miongoni mwa vitisho kwa usalama wa watoto nchini Yemen ni mashambulizi dhidi ya shule na hospitali, utumikishwaji vitani, ukatili wa kijinsia, na mabomu yaliyotegwa ardhini.

"UNICEF inakariri wito wake kwa pande zote za mzozo ili wajizuie kulenga maeneo yanayokaliwa na raia kama shule, hospitali na misikiti. UNICEF inaziomba pia pande hizi kusitisha utumikishwaji wa watoto vitani na kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa kulingana na kanuni za sheria ya kibinadamu na haki za binadamu"

Aidha Bwana Boulierac ameeleza kwamba mzozo wa kisiasa unarudisha nyuma nchi ya Yemen katika sekta za elimu, usalama wa chakula na afya, serikali ikikosa fedha za kuendeleza shughuli hizo. Amesema tayari Yemen ni miongoni mwa nchi ambapo watoto wameathirika zaidi na utapiamlo unaokumba asilimia 47 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5.