Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSMIL yatoa mapendekezo ya kuumaliza mzozo wa kisiasa Libya

UNSMIL yatoa mapendekezo ya kuumaliza mzozo wa kisiasa Libya

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Libya, Bernardino Leon, ametembelea miji ya Tobruk na Tripoli ili kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu jinsi ya kuongeza kasi ya mazungumzo ya amani, ambayo yamekuwa yakiendelea kwa majuma kadhaa, wakati hali ya usalama inapozidi kuzorota na kuhatarisha mazungumzo hayo.Mapendekezo hayo ni pamoja na kuunda serikali ya mseto ikiongozwa na rais, na Baraza la Urais likijumuisha makamu wake wawili na watu binafsi wasiokuwa na uhusiano na upande au kundi lolote, na ambao wanakubaliwa na pande zote na raia wote wa Libya. Pili, kuwe na bunge linalowawakilisha watu wote wa Libya

Tatu, kuwepo Baraza Kuu la kitaifa, likifuata mfano wa taasisi kama hizo katika nchi zingine, na mwisho, kuwepo Baraza la kuunda katiba.

Taarifa ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL, imesema kuwa mapendekezo hayo yametokana na mashauriano ya kina na pande zote husika nchini Libya, yakitilia maanani matakwa ya watu wa taifa hilo.

Taarifa hiyo imesema taifa la Libya limo hatarini kuingia katika machafuko zaidi na migawanyo, na hivyo kutoa mazingira ya kuenea kwa ugaidi ambao unatishia taifa hilo na ukanda mzima, na kwa hiyo halina muda wa kupoteza ili kufikia makubaliano yatakayorejesha usalama na ustawi, na kukomesha mateso kwa watu wake.